Karibuni NL Internet C@fe kwa huduma safi ya internet yenye kasi ya 5mbps kupandisha na kushusha.Tupo Tabata CCM,mkabala na kituo cha mafuta cha OILCOM.

Thursday, January 20, 2011

CHADEMA kisisikilizwe tena!

Ndugu wasomaji,

Tumeshuhudia jinsi nchi yetu ilivyokumbwa na vurugu za kisiasa jijini Arusha. Katika vurugu hizo damu ilimwagika. Ni wakati wa masikitiko makubwa kwa nchi yetu na vilevile ni wakati wa tafakuri na mafunzo muhimu. Je, ni nini kilichopelekea vurugu na kumwagika kwa damu?

Kimsingi mgogoro wa kisiasa ulisafirishwa kwenda Arusha. Chanzo chake ni halmashauri ya Hai. Katika halmashauri hiyo CHADEMA kiliwaorodhesha Mh. Lucy Owenya(MB) na Mh. Grace Kihwelu (MB) kuwa wapiga kura katika uchaguzi wa mwenyekiti wa halashauri hiyo. Kuorodheshwa kwao kulikipa CHADEMA nafasi kubwa ya kuweza kushinda uchaguzi huo. Tukumbushane tu, kuwa mwenyekiti wa CHADEMA Mh. Freeman Mbowe (MB) ni mjumbe katika halmashauri hiyo ya Hai. Kwa kutokuelewa sheria ipasavyo wajumbe kutoka CCM walipinga ushiriki wa wabunge hao wa CHADEMA katika uchaguzi wa mwenyekiti wa halmashauri. Hata hivyo wabunge hao wa CHADEMA waliruhusiwa kupiga kura na kumpa ushindi mgombea toka chama hicho. Hivi sasa halmashauri ya Hai inaongozwa na CHADEMA.

Tujifunze katika hili kuwa mwenyekiti wa CHADEMA anatambua kuwa wabunge wa viti maalum wanaweza kusajiliwa katika halmashauri fulani na kukipa chama chao "advantage" katika maamuzi yatakayofanywa katika vikao vya halmashauri hiyo. Katika kufahamu hili ndipo mwenyekiti huyu akawachukua wabunge wake hao wawili ili waweze kushinda uchaguzi. Pingamizi kutoka CCM kisheria halikuwa na nguvu yoyote.

Je, CHADEMA walifanya nini baada ya kukutana na changamoto huko Hai?

Walichokifanya CHADEMA ni kupinga uamuzi wa mkurugenzi wa halmashauri ya jiji la Arusha wa kumruhusu Mh. Mary Chatanda (MB) toka CCM kushiriki katika uchaguzi wa meya wa jiji la Arusha. Kigezo walichokitoa ni kwamba swala hilo si sahihi kisheria.

Tujiulize;
iwapo swala hilo si sahihi kisheria, ni kwanini Mh. Freeman Mbowe (MB) aliwasajiri Mh. Lucy Owenya(MB) na Mh. Grace Kihwelu (MB) toka CHADEMA kwenye uchaguzi wa Hai?
Je Mh. Freeman Mbowe (MB) alikuwa anajaribu kuvunja sheria?
Kwa vile waliopinga ushiriki wa wajumbe hao toka CHADEMA huko Hai ni wajumbe toka CCM, je CHADEMA inawatumia wajumbe wa CCM kuwajulisha sheria ya nchi inaruhusu vitu gani?
Iwapo CHADEMA hawajaridhishwa na maamuzi ya mkurugenzi wa Hai, je, ni sahihi kukataa maamuzi halali ya mkurugenzi wa jiji la Arusha kama majibu kwa mkurugenzi wa Hai?
Kwanini CHADEMA hawakuandamana Hai?

Kimsingi, maamuzi ya mkurugenzi wa jiji la Arusha ni maamuzi sahihi. Na wale wote waliowakatalia Mh. Lucy Owenya(MB) na Mh. Grace Kihwelu (MB) kushiriki uchaguzi wa mwenyekiti wa halmashauri huko Hai hawakuwa sahihi - na kwa vitendo, mwenyekiti wa CHADEMA amedhihirisha kulitambua hili.

Kitendo cha wajumbe kutoka CHADEMA kukataa kuchiriki uchaguzi kwa kisingizio cha kuwepo kwa Mh. Mary Chatanda (MB) kama mjumbe kingepelekea jiji la Arusha kushiindwa kupata meya, iwapo mkurugenzi angeendelea kusubiri wajumbe wafikie theluthi mbili. Je, ni kwanini CHADEMA waliona sawa kwa jiji la Arusha kushindwa kufanya uchaguzi wa meya ilhali wakijua kuwa maamuzi ya mkurugenzi kumruhusu mjumbe huyo toka CCM ni sahihi?

Hivi karibuni imeripotiwa kuwa CHADEMA kimeamua kumsajili Mh. Anna Komu (MB) kama mjumbe wa halmashauri ya jiji la Arusha. Maamuzi haya ni sahihi kisheria na yanathibitisha kuwa viongozi wa CHADEMA wanatambua kuwa Mh. Mary Chatanda (MB) ni mjumbe halali kwa sheria za nchi. Hata hivyo viongozi hao hawajaonyesha tabia ya kiung'wana ya angalau kuomba radhi kwa kuupotosha umma wa Arusha. Hii imedhihirisha kuwa viongozi hawa sio watu wawajibikaji.
Ninaamini CCM hawatajibu tukio hili kwa kuongeza mbunge mwingine wa viti maalum, kwa sababu kwa kufanya hivyo watakuwa wanaweka wananchi wa Arusha katika "political roller-coaster".

Wito: CHADEMA kisisikilizwe tena mpaka viongozi wake wakuu waliochochea vurugu zilizosababisha vifo huko Arusha (Dr. Wilbroad Slaa, Mh. Freeman Mbowe, Mh. Ndesamburo, ) watangaze kujiuzuru/ kuomba radhi umma kwa upotoshaji walioufanya.

Kwa nini kisisikilizwe?
CHADEMA kimekuwa chama ambacho viongozi wake wamekuwa wakifanya maamuzi bila kuyafanyia utafiti na tafakuri ya kutosha na inapodhihirika kuwa maamuzi hayo si sahihi wamekuwa wakitafuta lugha za "longolongo" za "ujanjaujanja".
1.Tumeshuhudia wakianzisha mchakato wa kutokumtambua Rais. Walipgundua kuwa uamuzi huo hautekelezeki/ hawawezi kuutekeleza, wakachezacheza na maneno bila kuwaomba radhi wananchi waliowapa support.
2. Tumeshuhudia viongozi wa CHADEMA wakisema kura zao za urais zimeibiwa na mgombea wao akiahidi kuleta vidhibiti vya kuhujumiwa kwenye uchaguzi. Mpaka sasa mgombea huyo wa CHADEMA hajatoa kidhibiti chochote wala hakuomba radhi kwa kutoa ahadi hewa.
3. Tumeshuhudia viongozi na waasisi wa CHADEMA wakiwanyima wanachama wao haki yao ya kikatiba ya kugombea nafasi za uongozi ndani ya chama hicho.
4. Tumeshuhudia viongozi wa CHADEMA wakiwanyima wanawake wanachama wa chama hicho kuchagua wabunge wao wa viti maalum.
5.Tumeshuhudia viongozi wa CHADEMA wakichangamkia kupeleka mchakato wa katiba bungeni. Walipokumbushwa na mwanazuoni Prof. Issa Shivji kuwa kufanya hivyo ni kuukabidhi mchakato huo kwa CCM wamekosa moyo wa kukiri upungufu kwenye mkakati wao huo/ angalau kumshukuru Prof. Shivji kwa angalizo hilo muhimu.
6. Tumeshuhudia viongozi wa CHADEMA wakitoa tamko la kutokuhudhuria mahakamani kusikiliza kesi waliyoshitakiwa. Viongozi wanaotegemewa kuonyesha mfano wa kutii utawala wa sheria wanaonyesha dharau kwa mahakama!
7.Leo tunashuhudia CHADEMA ikipeleka mbunge katika halmashauri ya jiji la Arusha jambo ambalo walipinga lisifanywe na CCM.

Je ni lini tutaanza kuwawajibisha viongozi wa CHADEMA?

Kama tunataka kuwaandaa viongozi wa CHADEMA kuwa viongozi wa taifa wawajibikaji, ni LAZIMA tuwawajibishe kuanzia sasa kwa maamuzi yao yote yanayokosa busara.

No comments:

Post a Comment